Mtaalamu wa maridhiano na utatuzi wa migogoro, Dkt. Dennis Mchunguzi, ameipongeza Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Othman Chande kwa kazi kubwa iliyofanywa kwa muda wa siku 153, akieleza kuwa haikuwa kazi rahisi bali ilihitaji umakini, weledi na uzalendo wa hali ya juu.
Aidha, amempongeza Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuunda tume hiyo, akisema hatua hiyo imeonyesha dhamira ya kweli ya kutafuta ukweli na kuimarisha misingi ya haki na amani nchini.Akizungumza baada ya kuisikiliza ripoti hiyo kwa kina, Dkt. Mchunguzi amesema, Nikiwa mtaalam na msomi mbobezi wa maridhiano na ujenzi wa amani, naweza kusema wazi kuwa ripoti hii imeandikwa kwa utaalam mkubwa, ikifuata viwango vya juu vya kitaaluma na kutekeleza ipasavyo hadidu za rejea.”
Hata hivyo, ameeleza masikitiko yake juu ya madhara yaliyotokea kufuatia matukio ya vurugu ya Oktoba 29, ikiwemo kupotea kwa maisha ya Watanzania, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali. Ameungana na Rais Samia kutoa pole kwa familia zilizoathirika na taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Dkt. Mchunguzi, ripoti hiyo ni nyenzo muhimu itakayosaidia taifa kusonga mbele kwa kujenga msingi wa haki, uwajibikaji na maridhiano ya kweli.
Akizungumzia hotuba ya Rais Samia wakati wa kupokea ripoti hiyo, alisisitiza kuwa msisitizo wake juu ya umoja wa kitaifa na mshikamano ni sahihi na wa wakati muafaka.
“Tunapaswa kuwa makini na maadui wasiolitakia mema taifa letu. Yaliyotokea yamelitia doa taifa, na hatupaswi kurudi huko tena,” amesisitiza.
Dkt. Mchunguzi pia alikaribisha msimamo wa Rais kuhusu kuanzishwa kwa mchakato wa maridhiano ya kitaifa, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuliponya taifa na kuweka msingi wa mabadiliko makubwa, ikiwemo kufikia Katiba Mpya.
Amefafanua kuwa kuchelewa kuanza kwa mchakato huo kulichangiwa na kusubiri ripoti ya tume, na sasa mapendekezo yaliyotolewa yatawezesha kuboresha na kuelekeza vyema hatua zinazofuata.
Aidha ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi za maridhiano. Tusipinge maridhiano, bali tuyakumbatie. Haya ndiyo yatakayotujenga upya kama taifa na kutupeleka katika hatua nyingine ya maendeleo. Kila mmoja anapaswa kuwa tayari kushiriki pale muda utakapofika.”
Kauli hiyo imekuja wakati taifa likianza tafakari mpya juu ya mustakabali wake, likiwa na matumaini kwamba kupitia maridhiano, linaweza kurejesha mshikamano, haki na amani ya kudumu.


0 Comments