SERIKALI YANUNUA VICHWA NANE VYA KUSAFIRISHIA KONTENA KUPITIA BANDARI KAVU YA KWALA PROF. KAHYARARA.


Na  Mwandishi Wetu,  Dar es salaam.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amesema  kuwa Serikali imenunua  vichwa nane vya Treni kati ya hivyo vichwa viwili vinatarajia kuwasili wakati wowote katika bandari ya Dar es Salaam ambavyo vitasaidia kusafirisha makasha kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda Bandari Kavu ya Kwala.

Kahyarara ameyasema hayo katika kikao cha wadau wa bandari kilichofanyika  jijini Dar es Salaam, kikao ambacho kimezikutanisha taasisi za TRC,TRA,TPA, Wizara ya Ulinzi, Uchukuzi, Mipango na Wadau kutoka sekta binafsi.

“ Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ambapo mpaka sasa imeshaagiza vichwa nane vya Treni ya kuondoshea mizigo ili viweze kusaidia kusafirisha Makontena kutoka  bandari ya Dar es Salaam kwenda Bandari Kavu ya Kwala, Amesema Kahyrara.

Kwa upande wake Meneja  wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus amesema Uhudumiaji wa mizigo katika  bandari hiyo umeongezeka  sana na  wanatarajia kufikia lengo walilojiwekea mwaka huu 2025/26 la kuhudumia tani  milioni 32 za Mizigo.


“Meli zinaendelea kuhudumiwa kama kawaida kwa ubora na kasi zaidi, kuna meli kubwa zinaendelea kutia nanga kwenye bandari ya Dar es Salaam na mizigo imeongezeka sana “ Amesema Gallus


Kwa upande wake mdau wa bandari Bw. Donald Tawalani ,Mkuu wa Kitengo cha huduma za makontena wa  kampuni  ya TEAGTL amesema mizigo imeongezeka hivyo ni muhimu wadau kuchukua mizigo na makontena yao kwa wakati ili bandari iweze kupata nafasi ya kuendelea kushusha mizigo mipya inayoletwa na meli.


Naye Mwenyekiti wa TATOA Bw. Rahim Dossa  ameomba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na Wakala wa Barabara (TANROAD) kujenga mizani katika eneo la Bandari Kavu ya Kwala ili kuondoa usumbufu  kwa madereva wa Malori.



Post a Comment

0 Comments