🔷️🔷️HATUNA MJOMBA WA KUTUSAIDIA, MAPITO YA OKTOBA 29 YATUIMARISHE- RAIS SAMIA

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kujifunza kutokana na ghasia za wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akibainisha kuwa hatma ya Tanzania ipo mikononi mwa Watanzania wenyewe na kukumbusha kuwa vurugu na ghasia haziwezi kubadilisha au kuleta suluhu ya changamoto za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

"Tufahamu kuwa hatma ya Tanzania ipo mikononi mwetu wenyewe, nguvu ya ushawishi wa makundi ya nje inasaidia kuvunja amani, kuvuruga usalama na kuvuruga nchi lakini kurudisha amani na usalama na kuijenga upya nchi yetu hufanyika kwa misingi ya misaada yenye masharti magumu ya kisiasa, kiuchumi na kibiashara. Kwahiyo tuwe makini kwamba watanzania ndio wajenga Tanzania wenyewe."


Rais Samia amebainisha hayo leo Alhamisi Aprili 23, 2026 Ikulu Jijini Dar Es Salaam mara baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa matukio ya ghasia za wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisema "tunapoibomoa Tanzania hakuna Mjomba wa kutusaidia, tutapata mikopo yenye masharti ili tuweze kujenga upya lakini wakati wa kubomoa tunaweza kupata misaada kirahisi kabisa." 


Rais Samia pia amewakumbusha watanzania kuhusu msemo maarufu wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela aliyesisitiza kuwa ili kuweza kukuwa hakuma budi kujifunza kutokana na matukio yanayofurahisha na yasiyofurahisha, akisema Tanzania imejifunza kutokana na ghasia za Oktoba 29 na kuwasihi Watanzania kushikamana ili kuimarika zaidi.


Post a Comment

0 Comments