Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kutenga na kuendeleza maeneo yote yaliyoombwa na Mama na Baba lishe, akimtaka kufanya kazi hiyo na Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuhakikisha kundi hilo linakuwa na maeneo mazuri ya kuweza kufanya shughuli zao.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Jumanne Aprili 21, 2026 Jijini Dar Es Salaam wakati wa kongamano la Kitaifa la Mama na Baba lishe, akimtaka Waziri Shemdoe pia kuhakikisha kundi hilo linakuwa na miundombinu bora ya kufanya kazi zao vizuri zaidi, akisisitiza kuwa upishi mzuri unaangazia zaidi nishati safi wakati wa kupikia pamoja na miundombinu rafiki kwa Mama na Baba lishe."Niagize pia kwa Wizara ya afya endeleeni kuimarisha mikakati ya utoaji wa elimu ya lishe na usalama wa chakula kwa Mama na Baba lishe ili kulinda afya ya walaji na kuimarisha viwango vya huduma zinazotolewa." Amesema Rais Samia.
Aidha Rais Samia pia ameiagiza Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu kwa kushirikiana na mamlaka za serikali na Taasisi za kijamii na sekta binafsi kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa mitaji ya Mama na Baba lishe ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija.
Rais Samia pia ametoa maagizo kwa Wizara ya fedha kwa ushirikiano na mamlaka nyingine za serikali kuweka mazingira rafiki ya kisera na kisheria ili wafanyabiashara ndogondogo ikiwemo Mama na Baba lishe waweze kunufaika ipasavyo na huduma za kifedha zinazotolewa nchini pamoja na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Awali wakati wa risala ya Umoja wa Mama lishe Tanzania, Katibu wa Umoja huo Bi. Julieth Malata alimuomba Rais Samia kufanya maboresho ya masoko ya Kigamboni Feri, Buguruni na Magomeni ya Jijini Dar Es Salaam, Sabasaba la Mkoani Mwanza, Kilombero Arusha, Mlango wa Chuma Tanga pamoja na masoko mengine nchini huku pia wakiomba miundombinu rafiki kwa masoko ya ghorofa kwani kwenye Sekta ya Mama na Baba lishe wapo pia wajasiriamali wenye ulemavu.


0 Comments