Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ingewezekana siku kurudi nyuma, yaliyotokea Oktoba 29, 2026 asingetamani yatokee na historia ijiandike upya ili kufuta doa ambalo Tanzania iliingia kutokana na Ghasia zilizofanyika wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akihimiza Watanzania kudumisha amani na umoja ili kutoruhusu kuvurugwa na maadui wa Tanzania.
Rais samia ameyasema hayo leo Alhamisi Aprili 23, 2026 Ikulu Jijini Dar Es Salaam, mara baada ya kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba mwaka jana, akiwashukuru Watanzania kwa kutoendelea na matukio ya vurugu licha ya hamasa kubwa iliyokuwa ikitolewa na baadhi ya watu kwenye Mitandao ya kijamii pamoja na imani yao kubwa kwa serikali wakati wakisubiri ripoti hiyo ya matukio ya Oktoba 2025.
"Walioumizwa na tukio lile ni sisi Watanzania, ni sisi tuliopoteza watoto wetu, ndugu zetu, jamaa na marafiki zetu. Kwa hali yoyote ile walioathirika ni watanzania kwa ujumla wetu. Haiwezekani mtu mwingine asiye Mtanzania awe na uchungu zaidi kuliko sisi watanzania. Walau kungekuwa na uwezekano tunatamani siku zirudi nyuma yaliyotokea Oktoba 2025 yawe hayakutokea na historia ijiandike upya ili tuweze kufuta doa tuliloingia." Amesema Rais Samia.
Rais Samia kadhalika amerejea falsafa ya Muasisi wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akibainisha kuwa nchi ikiwa na umoja na mshikamano, itakuwa ngumu kuinyonya na kuitawala kisiasa au kiuchumi, akisema Mataifa mengi yenye rasilimali yamehujumiwa na kuingizwa kwenye migogoro ili kurahisisha uvunaji wa rasilimali zilizopo kwenye Mataifa hayo, akisema migogoro imekuwa sababu ya umaskini wa Afrika.






0 Comments