Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amesema katika siku za hivi karibuni ataunda tume ya maridhiano itajayojumuisha wadau wote muhimu kwaajili ya kusimamia na kuongoza majadiliano na maridhiano ili kuziba mianya na migawanyiko iliyopo kwa lengo la kurejesha umoja na ushirikiano wa Kitaifa.
"Naomba nikumbushe kuwa nia ya kuwa na Tume ya maridhiano ilikuwepo kabla hata ya matukio ya Oktoba 29, 2025 na ni moja ya ahadi yangu niliyoahidi kutekeleza ndani ya siku 100 za kwanza, hata hivyo ghasia za Oktoba 25 zimechelewesha utekelezaji wa ahadi hiyo kwakuwa hata hadidu za rejea za wakati ule zitapaswa kubadilika."Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 23, 2026 Ikulu Jijini Dar Es Salaam mara baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29, 2025, akisema baada ya Tume kuwasilisha ripoti yake, ndiyo itakayoelekezwa kwenye mchakato wa kurekebisha Katiba ya nchi.
Rais Samia pia amesema kwakuwa ripoti ya Jaji Mstaafu Mohamed Othman Chande imeeleza kuwepo kwa viashiria vya jinai, serikali itaunda chombo maalumu cha upelelezi kwaajili ya kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande ambapo pamoja na mambo mengine kitatakiwa kubaini waliopanga, kuratibu na kufadhili matukio ya uhalifu na vurugu za Oktoba 29, 2025 ikiwemo wale waliokuwa wakifanya matukio ya wizi na unyang'anyi pamoja na kushughulikia vifo vya watoto na wale ambao wanadaiwa kutekwa na taarifa zao bado hazijapatikana.
Rais Samia vilevile ametangaza kuwa serikali itaweka utaratibu wa kugharamia matibabu ya majeruhi wa ghasia za Oktoba 29, vifaa saidizi na viungo bandia kwa waliopata ulemavu wa kudumu pamoja na kutoa usaidizi kwa wafanyabiashara wadogo wadogo waliopata hasara kutokana na ghasia hizo za wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.


0 Comments