🔷️🔷️WALIOFANYA GHASIA OKTOBA 29 WALIPEWA MAFUNZO NA MALIPO- JAJI CHANDE

 

Tume ya kuchunguza matukio ya Uvunjifu wa amani ya Wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imesema imepata ushahidi usio wa shaka kuwa matukio ya Oktoba 29 yalipangwa, kuratibiwa, kufadhiliwa na kutekelezwa na watu waliopata mafunzo.

Akiwasilisha ripoti ya Tume hiyo kwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Aprili 23, 2026, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, amesema waratibu wa ghasia hizo walitumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuwatumia Vijana na watu wasiokuwa na ufahamu wa kutosha na waliokata tamaa, wakiratibu pia matukio hayo kufanyika kwa wakati mmoja katika maeneo tofauti ili kuwatawanya na kulichanganya Jeshi la Polisi.


"Mhe. Rais taarifa na ushahidi unathibitisha kuwa watu waliokuwa wakizunguka maeneo mbalimbali kama Vyuoni na Masokoni, wakishawishi na kuwaandikisha watu kushiriki katika ghasia za wakati na baada ya uchaguzi Mkuu."


" Watoto wanaoishi katika mazingira magumu, waendesha pikipiki na wajasiriamali wadogo walieleza pia kwamba walipewa fedha kati ya Shilingi 10,000 hadi Shilingi 50,000, waliahidiwa ajira na maisha bora na zaidi kuanzia tarehe 12 Oktoba, 2025 hadi  tarehe 28 Oktoba 2025 waliwekwa pamoja, kupewa mafunzo, kuandaliwa na kuhamasishwa kuwa sehemu ya kuanzisha na kushiriki ghasia siku hiyo." Amesema Jaji Chande.


Kulingana na Mwenyekiti huyo, imebainika pia kwamba walioshawishiwa ndiyo waliokuwa washiriki zaidi wa ghasia hizo huku wahusika wakuu na waratibu wakiwa hawapo kwenye matukio hayo suala lililosababisha kutokamatwa kwao na zaidi wakikamatwa wananchi wa kawaida na wafuata mkumbo.


Post a Comment

0 Comments