Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025 Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema kulingana na sheria na uchambuzi wa Tume hiyo, kilichotokea Oktoba 29, 2025 hayakuwa maandamano ya amani bali ilikuwa ghasia zilizoambatana na matukio ya uvunjifu wa amani.
Jaji Chande amebainisha hayo leo Aprili 23, 2026 mbele ya Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akisoma ripoti ya uchunguzi wa Tume hiyo Ikulu Jijini Dar Es Salaam, akisema hitimisho hilo limetokana na sababu kadhaa ikiwemo kutozingatiwa kwa Katiba ya Tanzania na sheria za nchi zinazotaka Notisi kwa Jeshi la Polisi kwa wanaotaka kuandamana.Jaji Chande pia amesema yanayoitwa maandamano ya Oktoba 29 hayakuwa maandamano kwani sheria pia zinatoa haki kwa kila mtu kushiriki katika uchaguzi Mkuu na ghasia hizo zilipangwa siku ambayo ilishatangazwa kisheria kuwa siku ya uchaguzi Mkuu suala ambalo lilisababisha kupokwa kwa haki ya kisheria kwa wananchi kuweza kushiriki uchaguzi.
"Washiriki wa ghasia za wakati na baada ya uchaguzi walibeba silaha za aina mbalimbali ikiwemo mawe, nondo, mikuki, sururu, fimbo, rungu, viberiti, visu, bunduki, manati, kombeo, rato na mapanga jambo ambalo haliruhusiwi kisheria katika maandamano ya amani." Amesema Jaji Chande.
Mwenyekiti huyo pia ametaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na sheria na taratibu za Kimataifa, kikanda na Kitaifa kutoruhusu maandamano yenye kusababisha taharuki kwenye jamii, kuhatarisha usalama wa Taifa, kusababisha uharibifu na kuhatarisha maisha ya watu wengine.


0 Comments