Ⓜ️πŸ›‘πŸ›‘πŸ›‘DKT. YONAZI AKAGUA MAANDALIZI YA WIKI YA KITAIFA YA WATU WENYE ULEMAVU MWANZA


Na Mwandishi Wetu - Mwanza


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, amekagua maandalizi ya Wiki ya Kitaifa ya Watu Wenye Ulemavu - 2026 yanayoendelea Jijini Mwanza.

Dkt. Yonazi amekagua maeneo mbalimbali yatakayotumika katika maadhimisho hayo, ikiwemo Viwanja vya Nyamagana, Jiji la Mwanza, ambapo shughuli kuu za wiki hiyo zinatarajiwa kufanyika.

Wiki hiyo ya Kitaifa inatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe *27 Novemba hadi 3 Desemba 2026*, na kaulimbiu yake ni *“SAUTI YETU, MAONI YETU, MUSTAKABALI WETU.”*

Akiwa katika ukaguzi huo, Dkt. Yonazi amepata taarifa za maandalizi kutoka kwa kamati ya maandalizi, ikiwemo maandalizi ya viwanja, mabanda ya maonesho, ulinzi na usalama, huduma za afya, pamoja na mipango ya kuwapokea wageni na washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Amesisitiza umuhimu wa maandalizi kukamilika kwa wakati na kwa ubora, ili wiki hiyo iweze kuwanufaisha kikamilifu watu wenye ulemavu.


"Wiki hii iwe yenye manufaa na mafanikio kwa watu wenye ulemavu na itumike kama fursa nzuri ya kukuza uchumi pia kupitia maonesho ya shughuli za wenye Ulemavu, serikali tutaendelea kuunga mkono jitihada zenu kuhakikisha zinazaa matunda," alisema Dkt. Yonazi 


Aidha, Dkt. Yonazi amewataka wadau wote wanaohusika na maandalizi kuongeza ushirikiano na kuhakikisha miundombinu yote, hususan inayowahusu watu wenye ulemavu, inakuwa rafiki na yenye kuwafikia wote.


Kwa upande wake, uongozi wa Mkoa wa Mwanza umemhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa maandalizi yako katika hatua nzuri na kwamba Mkoa uko tayari kuupokea na kuandaa wiki hiyo ya Kitaifa.


Wiki ya Kitaifa ya Watu Wenye Ulemavu huadhimishwa kila mwaka kuelekea Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, Desemba 3.





Post a Comment

0 Comments