Na Mwandishi wetu, Dar esalaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Abdallah Mitawi, ameitaka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo kwa kuzingatia viwango vya usalama, ubora na ufanisi, ili Tanzania iendelee kuwa na anga salama na sekta yenye ushindani kikanda na kimataifa
Bw. Mitawi ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya TCAA, ambapo alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na maendeleo ya sekta ya anga nchiniAmesema sekta ya anga ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuwezesha usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma kwa haraka na kwa ufanisi. Kwa msingi huo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika usalama, teknolojia, miundombinu na rasilimali watu wenye ujuzi wa kisasa, huku akipongeza hatua zinazochukuliwa na TCAA kuhakikisha anga la Tanzania linakuwa salama na kuwataka kuimarisha mifumo ya udhibiti, usimamizi na utoaji wa huduma kwa wadau wa sekta hiyo
Katika ziara hiyo, Bw. Mitawi amejionea maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) na kutembelea Kituo cha Kudhibiti Usafiri wa Anga (ACC) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere pamoja na kituo cha rada ambapo ameridhishwa na namna shughuli za usafiri wa anga zinaendeshwa kwa usalama,ufanisi na kuzingatia viwango vya kimataifa
Vilevile, Naibu Katibu Mkuu ameitaka TCAA kujiandaa mapema kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwemo mvua kubwa zinazotarajiwa katika kipindi kijacho na kusisitiza umuhimu wa Mamlaka kuwa na mifumo madhubuti ya usalama, mawasiliano na uendeshaji wa shughuli za anga ili huduma ziendelee kutolewa kwa usalama na ufanisi katika mazingira yote
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Dkt. Jabiri Bakari, amemueleza Naibu Katibu Mkuu hatua mbalimbali zinazotekelezwa na Mamlaka hiyo katika kuimarisha usalama wa anga, kuboresha huduma, kuendeleza rasilimali watu na miundombinu, pamoja na kuhakikisha usimamizi wa shughuli za anga unazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
















0 Comments