Na Sheila Ahmadi, Geita
Maisha ya wastaafu nchini yameendelea kuboreshwa kupitia maboresho yanayofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ikiwamo ongezeko la pensheni ya chini kutoka Sh100,000 hadi Sh250,000 kwa mwezi.
Hatua hiyo, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 150, imeelezwa kuwa sehemu ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku PSSSF ikiendelea kuboresha huduma kwa wanachama na wastaafu.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alisema hayo alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Amesema kuwa maboresho hayo hayajaishia katika ongezeko la pensheni, bali yameenda sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wastaafu, ikiwamo uhakiki kwa njia ya kidijitali.
“Zamani mstaafu kutoka Kakonko au Chato ilimlazimu kusafiri hadi Dar es Salaam au Dodoma kwa ajili ya uhakiki. Leo, mateso hayo yamebakia historia,” alisema Waziri Sangu".
Aidha Waziri Sangu, PSSSF imeboresha mifumo yake ya TEHAMA na kuwezesha wastaafu kuhakikiwa wakiwa katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama.
Vilevile mfuko huo umeendelea kuboresha utoaji wa mafao kupitia kaulimbiu ya “Tunalipa Jana”, inayolenga kuhakikisha mafao ya wastaafu yanalipwa kwa wakati na kupunguza urasimu.
Katika hatua nyingine ameongeza kuwa pensheni ya kila mwezi pia inalipwa kabla ya tarehe 25, hatua ambayo imeendelea kuwapa uhakika wastaafu katika kupanga maisha yao ya kila siku.
Hata hivyo mafanikio hayo yanaenda sambamba na ukuaji wa thamani ya mfuko, ambayo imeongezeka kutoka Sh trilioni 7.4 wakati Rais Samia anaingia madarakani hadi Sh trilioni 16.96 kwa sasa.
ongezeko hilo linaonyesha namna PSSSF ilivyoimarisha usimamizi wa fedha za wanachama na wastaafu, huku ikiendelea kuwekeza katika kuboresha huduma.
Pia Mbali na huduma za mafao, alisema PSSSF imekuwa ikitoa elimu kwa watumishi kwa kushirikiana na waajiri kote nchini, kwa lengo la kuwaandaa watumishi kiuchumi na kisaikolojia kabla ya kustaafu.
maandalizi hayo yanakusudia kuhakikisha mtumishi anapoondoka katika utumishi wa umma anaendelea kuwa na maisha yenye matumaini na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya baada ya kustaafu.
Kupitia hatua hiyo PSSSF imeendelea kujenga mfumo unaolenga kumlinda mtumishi wa umma katika kipindi cha ajira na baada ya kustaafu, huku maboresho ya pensheni, malipo ya mafao na huduma za kidijitali yakibeba sehemu muhimu ya mabadiliko hayo.


0 Comments